Thatcher aaga dunia
London Uingereza -
Waziri mkuu wa zamani wa
Uingereza Margaret Thatcher ambaye alikuwa akijulikana kama "Iron Lady"
kwa ukakamavu wake ambaye amezifanyia marekebisho siasa za kizazi cha
Uingereza amefariki dunia baada ya kupigwa na kiharusi leo akiwa na umri
wa miaka 87. Mengi zaidi na Mohammed Dahman.
Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza na Waziri Mkuu David Cameron
wameongoza katika salamu za rambi rambi kwa waziri mkuu huyo wa kwanza
mwanamke nchini Uingereza, muumini mashuhuri kabisa wa sera za mrengo wa
kulia na mtu muhimu wakati wa Vita Baridi.
Msemaji wa familia ya Thatcher amekaririwa akisema "kwa masikitiko
makubwa Mark na Carol Thatcher (watoto wa marehemu) wanatangaza kwamba
mama yao Bi. Thatcher amefariki kwa utulivu baada ya kupigwa na kiharusi
leo asubuhi."
Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye aliiongoza Uingereza kuanzia mwaka
1979 hadi mwaka 1990 alikuwa akikabiliwa na maradhi ya kupoteza
kumbukumbu na mara chache amekuwa akionekana hadharani katika miaka ya
hivi karibuni.
Mara ya mwisho alilazwa hospitalini hapo mwezi wa Disemba mwaka jana kwa
ajili ya operesheni ndogo ya kuondowa uvimbe kwenye nyonga yake.
Kiongozi huyo wa zamani wa chama cha Conservative amebakia kuwa waziri
mkuu pekee mwanamke katika historia ya Uingereza na kiongozi aliekaa
mfululizo kwa muda mrefu kabisa katika makao makuu ya serikali ya
Downing Street katika karne ya 20.
Binti yake wakati fulani aliwahi kusema kwamba waziri mkuu huyo wa
zamani inabidi akumbushwe mara kwa mara kwamba mume wake Denis amefariki
mwaka 2003.
Thatcher alitakiwa na madaktari kuacha kuhutubia hadharani muongo mmoja
uliopita baada ya kukumbwa mara kadhaa na kiharusi kidogo.
Kasri la Kifalme la Uingereza Buckingham Palace limetowa taarifa ikisema
kwamba Malkia amesikitishwa kusikia habari za kifo cha Thatcher na
kwamba atatuma ujumbe binafsi wa masikitiko kwa familia.
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amekatisha ziara yake katika nchi
kadhaa za Ulaya na amesema kwamba kwa huzuni kubwa amepokea habari za
kifo cha Bibie huyo na kwamba wamempoteza kiongozi adhimu,waziri mkuu
adhimu na Muingereza adhimu.Ameongeza kusema kwamba Thatcher "
ameitumikia nchi yake vizuri sana,ameiokoa nchi yake na ameonyesha
ushujaa mkubwa sana katika kufanya hivyo.Watu watakuwa wanajifunza juu
ya kile alichokifanya na mafanikio yake kwa miongo kadhaa inayokuja na
yumkini hata kwa karne kadhaa.Hiyo dio haiba yake.”
Michael Howard kiongozi wa chama cha Conservative kuanzia mwaka 2003
hadi mwaka 2005 amekiambia kituo cha televisheni cha Sky kwamba ni
habari za kuhuzunisha sana kwani alikuwa ni mashuhuri sana katika siasa
za Uingereza.
Howard anaamini kwamba Thatcher ameiokoa nchi yao, ameubadili uchumi wa
nchi hiyo na anaamini kwamba ataingia katika historia akiwa kama
mmojwapo wa mawaziri wao wakuu walio adhimu kabisa.
Wafuasi wa sera za mrengo wa kulia wanampongeza mama huyo kwa kuitowa
Uingereza kwenye msononeko wa kiuchumi lakini wafuasi wa mrengo wa shoto
wanamshutumu kwa kuving'owa viwanda vilivyokuwepo tokea enzi za jadi na
kuvunja kiini cha mshikamano wa jamii.
Katika jukwaa la kimataifa alijenga uhusiano maalum na Rais Ronald
Reagan wa Marekani jambo ambalo limesaidia kuuangusha ukomunisti katika
Muungano wa Kisovieti.Pia alikuwa akipinga vikali uhusiano wa karibu wa
Ulaya.
Thatcher alizaliwa akiwa anajulikana kwa jina la Margaret Hilda Roberts
hapo tarehe 13 Oktoba mwaka 1925 katika mji wa sokoni wa Grantham
mashariki ya Uingereza akiwa ni binti wa muuza duka la vyakula na bidhaa
ndogo ndogo.
Baada ya kumaliza shule na kujipatia shahada yake ya Kemia katika Chuo
Kikuu cha Oxford alifunga ndoa na mfanyabiashara Denis hapo mwaka 1951
na miaka miwili baade walibarikiwa watoto mapacha Carol na Mark. Mara ya
kwanza alichaguliwa katika bunge hapo mwaka 1959 na alichukuwa nafasi
ya waziri mkuu wa zamani Edward Heath kama kiongozi wa chama cha
upinzani cha Conservative hapo mwaka 1975 kabla ya kuwa waziri mkuu
miaka minne baadae.
Haiba yake ya kudumu inaweza kuelezwa kwa muhtasari kuwa ya "Thatcherism
" yaani mkusanyiko wa sera ambapo wafuasi wake wanasema zimeendeleza
uhuru wa mtu binafsi na kusambaratisha mgawanyiko wa kitabaka ambao
ulikuwa umeipasuwa Uingereza kwa karne kadhaa.
Hata hivyo kushinikiza sera zake kuliiweka serikali yake katika
mapambano kadhaa magumu.Itakumbukwa wakati Argentina ilipovivamia visiwa
vya Falklands vilivyoko chini ya himaya ya Uingereza hapo mwaka 1982,
Thatcher alituma vikosi na meli za kivita na kuvikombowa katika kipindi
cha miezi miwili.
Na hadi sasa visiwa kisiwa cha Falklands kimekuwa na mzozo kati ya Argentina na Uingereza nani ni mmiliki halali wa ene hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni