Alhamisi, 25 Aprili 2013

world malaria day

 siku ya malaria duniani

Huku dunia ikiadhimisha siku ya Malaria  hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa ujumbe na kusema kuwa bado ugonjwa huo ni tishio  kwa nchi maskini hususan barani Afrika, ambako mamilioni ya watu wanashindwa kujikinga dhidi ya Malaria. 

Isitoshe,Bwana Ban amesema barani Afrika kila dakika mtoto mmoja anafariki dunia kutokana na ugonjwa huo na kwamba mifumo dhaifu ya ufuatiliaji inakwamisha uwezo wa serikali na shirika la afya duniani, WHO kupata taarifa za kina kuhusu maeneo mapya yenye ugonjwa huo na mabadiliko ya mwenendo wa ugonjwa huo. Amesema usugu wa vijidudu vya Malaria dhidi ya dawa za kunywa na hata katika vyandarua vyenye viuatilifu, unafanya hali kuwa mbaya zaidi kuweza kutokomeza ugonjwa huo na hivyo kutishia uhai na maendeleo.

 Kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani kwa Mwaka 2013; Wekeza kwa siku za baadaye. Shinda Malaria.

Bwana Ban amesema  ameisihi jumuiya ya kimataifa ikiwemo wanasiasa katika nchi zinazotishiwa na ugonjwa huo kuwekeza fedha na kuendeleza azma yao ya kuhakikisha kila mwananchi anaweza kujikinga dhidi ya Malaria.

 Nchi 50 kati ya nchi 99 zinazoendelea kufanya vyema ili kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia kwa mwaka 2015 kwa kupunguza vifo kwa asilimia 75%. Jambo hili linawezekana ikiwa kama kutakuwepo na udhibiti zaidi wa ugonjwa wa Malaria, kwa kuwa na vifaa vizuri vya kuchunguza pamoja na dawa zinazotibu Malaria.

Malaria ni ugonjwa unaoendelea kupukutisha maisha ya watu wapatao 660,000 kutoka kila kona ya dunia, wengi wao ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano, na mama wajawazito wanaoishi Kusini mwa Jangwa na Sahara.

Zaidi ya watu millioni 200 wanashambuliwa na ugonjwa wa Malaria. Kesi nyingi hazipimwi wala kupatiwa tiba muafaka. Dawa zisizo na viwango zinasababisha usugu, jambo ambalo linaweza kukwamisha jitihada za Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni