Jumatatu, 10 Desemba 2012

mkataba wa Kyoto


 

Hatimaye mkutano wa kujadili mabadiliko ya hali ya hewa mjini Doha umeafiki kurefushwa Mkataba wa Kyoto hata baada ya  nchi ya  Urusi kujaribu kuyapinga mafikiano hayo.


Wajumbe katika mkutano huyo, walijikaza kisabuni ili kupata suluhu katika hoja ambayo hakika ilikuwa ya dharula.


Maji taka
Mkutano huu uliwaleta pamoja wajumbe zaidi ya 17,000 kutoka nchi 200 duniani, uliafiki  kurefushwa Mkataba wa Kyoto unaodhibiti uzalishaji gesi za nyumba ya kioo hadi mwaka 2020.  

Isitoshe,nchi 27 za Umoja wa Ulaya, Australia na Uswisi na nchi nyingine nane zenye maendeleo ya viwanda zimekubali kushikamana na makubalino ya kuzuia uzalishaji wa gesi hizo hadi mwaka 2020.

Hata hivyo,Marekani imekataa kutia saini Mkataba wa Kyoto.

Pia  makubaliano hayo hayazihusishi nchi zinazochafua kwa kiasi kikubwa mazingira kama China na India.

Katika hotuba yake , Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon,aliunga mkono hatua hiyo na kuzisitiza kuwa ni jukumu la, serikali kwa ushirikiano na wananchi, makundi ya kibiashara na jumuiya za kiraia, kuchukua hatua zaidi.  

Zaidi ya hayo, aliongeza kuwa, ili kuhakikisha dunia inakuwa salama kutokana na matumizi ya gesi chafu ni lazima nchi wanachama zikubaliane na mpango wa kuhakikisha zinapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya Carbon ili kunusuru tabaka la hewa.




 Mkutano huo ni wa 18 na  unafanyika kwa mara ya kwanza katika eneo la Ghuba ya Uajemi . Kwenye sherehe za ufunguzi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Maite Nkoana-Mashabane amekabidhi uongozi wa COP kwa Naibu Waziri Mkuu wa Qatar, Abdullah bin Hamad al-Attiyah.


Wajumbe kwenye mkutano huo walionyesha kudoridhika na kugawanyika kuhusu azimio la Kyoto la mwaka 1997 linalozitaka nchi tajiri kuzilipa fidia nchi masikini zinazoathirika na gesi za sumu zinazotoka katika viwanda vyao. Mkataba wa Kyoto ambao ulianza kufanya kazi mwaka 2005, haujawa na athari kubwa katika suala la kupunguza uchafuzi wa mazingira kwani nchi kubwa kama Marekani na China zimeshindwa kutekeleza azimio hilo.

Marekani ilikataa kusaini mkataba huo nayo China ikakataa kuutekeleza licha ya kuusaini. Canada kwa upande wake ilijiondoa kwenye mkataba wa Kyoto mwaka jana.
Mkataba wa Kyoto unazitaka nchi wanachama hasa zile zenye viwanda vingi kupunguza matumizi ya Carbon pamoja na kutoa fedha za kutosha kwa nchi zinazoendelea ili kuzipa uwezo wa kukabiliana na uharibifu wa tabaka la hewa.

Wataalamu wa masuala ya mazingira wanasema kuwa iwapo nchi za Marekani, Canada, China, Urusi na Uingereza hazitakubali kwa sasa kupunguza matumizi ya Carbon basi dunia hasa nchi zinazoendelea zinakabiliwa na hatari kubwa ya kukumbwa na hali joto ambayo ni hatari kwa mazingira na viumbe hai.

Mkataba huu ulitarajiwa kukamilika baadaye mwaka huu.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni